9 Aprili 2025 - 21:17
Source: IQNA
Masharti ya Tawakkul yanaathiri tabia ya mwanadamu

Baadhi ya imani za kidini si tu kwamba zinakuwa masharti ya kiakili ya Tawakkul, bali pia huathiri mwenendo na tabia ya mwanadamu.

Kwa mfano, mtu anapofahamu sifa za Mwenyezi Mungu, anaweza kuonesha subira, ujasiri, na heshima katika vitendo vyake anapofuata haki.
Baadhi ya maarifa ya mtu kuhusu ulimwengu na Mwenyezi Mungu humpelekea kutokuwa na matumaini kwa viumbe na kumuelekea Mola wake wa haki. Kwa hakika, utambuzi huu humwelekeza mwanadamu katika njia ya kumuwezesha kumtegemea kwa dhati. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ametuongoa kwenye Njia zetu." (Surat Ibrahim, Aya ya 12)

Imani hizi humhamasisha mtu kuifuata njia ya uongofu. Anapoingia katika njia hii, changamoto na mitihani hujitokeza, lakini mtu anayemtegemea Mwenyezi Mungu (yani mwenye Tawakkul) hukabiliana nazo kwa subira, heshima, ujasiri, na ucha Mungu.

Kwa hivyo, inaweza kusemwa kwamba masharti ya kiakili yanayohusiana na dhamira ya mtu hupelekea utekelezaji wa kiutendaji wa Tawakkul.

Katika Surah At-Tawbah, Mwenyezi Mungu anazungumza kwanza juu ya huruma na shauku ya Mtume Mtukufu (SAW) ya kuwaongoza watu.
"Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma." (Surat At-Tawbah, Aya ya 128)

Kisha katika aya inayofuata, inabainishwa kuwa mtu asifikirie kuwa juhudi na huruma za Mtume (SAW) kwa watu ni kwa sababu anawahitaji. Kwani hata kama watu wote watamkataa, bado Mwenyezi Mungu yuko pamoja naye.
Mwenyezi Mungu, ambaye huendesha na kulinda mfumo mpana wa uumbaji, ana uwezo wa kumhifadhi mwanadamu chini ya rehma Zake: "Basi wakigeuka, wewe sema: Mwenyezi Mungu ananitosheleza. Hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mimi namtegemea Yeye, na Yeye ndiye Mola Mlezi wa Kiti Kikuu cha Enzi.." (Surat At-Tawbah, Aya ya 129)

Katika Surah Al-Ahzab, Aya ya 48, tunasoma:
"Wala usiwat´ii makafiri na wanaafiki, na usijali udhia wao. Nawe mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa."

Kuyadharau maudhi na njama za makafiri na wanafiki, kupinga matakwa yao, na kutokukatishwa tamaa na vitendo vyao, kunahitaji Tawakkul, kwa kuwa Yeye ndiye Msaidizi na Mlinzi bora.
Kwa hakika, misingi ya kiutendaji ya Tawakkul hii ni subira, heshima, na ujasiri wa kutokuogopa matokeo.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha